Post Code : P.O BOX 3000 - 80100 MOMBASA
July 2024
2:0 minute
Exam code: 405745
1. Andika jina lako na nambari yako ya mtihani katika nafasi ulizoachiwa hapo juu.
2. Tia sahihi yako kisha uandike tarehe ya mtihani katika nafasi ulizoachiwa hapo juu.
3. Jibu maswali yote.
4. Majibu yote yaandikwe katika nafasi ulizoachiwa katika kijitabu hiki cha maswali.
5. Majibu yote lazima yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili.
6. Watahiniwa ni lazima wahakikishe kwamba kurasa zote za karatasi hii zimepigwa chapa sawasawa na kuwa maswali yote yamo.
1 | 2 | 3 | 4 | Total |
---|---|---|---|---|
Jibu maswali yote
UFAHAMU:( Alama 15)
Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.
Meli alipokivuka kizingiti cha lango la shule ya kitaifa ya Tungambele alikuwa na azma ya kusoma kwa bidii ili kuinukia kuwa kijana wa kutegemewa na jamii yake. Alikuwa kalelewa katika familia yenye pato wastani. Akasoma kwa juhudi za wazazi wake hadi darasa la nane alipokwangura alama za kumwezesha kujiunga na shule hii ya kifahari. Meli alijua kwamba alikuwa mwanagenzi, si katika masomo ya shule ya upili tu, bali pia katika maisha ya jijini ambamo shule hii ilipatikana. Kwa kweli hii ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kutia guu kwenye jiji hili ambalo habari zake akizisoma, ama katika magazeti machache yaliyowahi kufika kijijini, au kupitia somo la Elimujamii. Hata hivyo, Meli hakuwa mtu wa kuogopa au kunywea machoni mwa changamoto. Alijiambia kwamba kwa vyovyote vile atapambana na maisha haya mapya.
Saa mbili kamili asubuhi ilimpata Meli kapiga foleni katika afisi ya kuwasajili wanafunzi wageni. Wasiwasi wa aina fulani ulianza kumnyemelea alipotazama hapa na pale bila kuona dalili ya mja yeyote aliyemfahamu. Alijihisi kama yule kuku mgeni ambaye mwalimu wake alishinda kuwaambia kuwa hakosi kamba mguuni. Hata hivyo aliupiga moyo wake konde na kujiambia kuwa kuja kwake hapa kulitokana na juhudi zake mwenyewe na katu hatauruhusu ugeni wa mazingira kuifisha ari yake ya masomo.
Usajili ulikamilika, naye Meli na wenzake wakajitosa katika ushindani wa kimasomo jinsi waogeleaji wajitumbukizapo kidimbwini wakapiga mbizi, baadhi wakiambulia ushindi na wengine wakifedheheka kwa kushindwa. Meli na wenzake walibainikiwa kwamba wote walikuwa mabingwa kutoka majimbo na wilaya zao. Ilimbidi kila mmoja wao kujikakamua zaidi ili kuelea katika bahari hii ya ushindani. Muhula wa kwanza ulishuhudia kishindo cha Meli kubwagwa chini na majabali wenzake. Alijipata miongoni mwa wanafunzi kumi wa mwisho; au kama alivyozoea kuwatania wenzake katika shule ya msingi, “wanafunzi kumi bora kuanzia mwisho”! Hili lilimwatua moyo Meli na kumfanya kutahayari. Alifika kwao amejiinamia kama kondoo aliyeumia malishoni. Akawataka wazazi wake wambadilishie shule lakini wakakataa.
Muhula wa pili na wa tatu mambo yalikuwa yaleyale. Meli akahisi kama askarijeshi aliyeshindwa kabisa kutambua mbinu za kuwavizia maadui. Akaona kwamba njia ya pekee ni kujiunga na wenzake kama yeye katika vitendo vya utundu kama vile kuvuruga masomo kwa kupiga kelele darasani, kupiga soga bwenini na hata kuvuta sigara. Mwanzoni alichukia vitendo hivi lakini alimeza mrututu akisema kwamba ndiyo njia ya pekee ya kujipurukusha na aibu. Wazazi wa Meli hawakusita kutambua mabadiliko katika hulka ya mwanao. Wakajaribu kumshika sikio nyumbani lakini akawa hasikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini. Wakawahusisha wataalamu wa ushauri nasaha ambao waliwaambia kuwa Meli hakuwa na tatizo lolote la kuyadumu masomo. Kile alichokosa ni kujiamini tu.
Wazazi wa Meli waliona kuwa ni muhimu kuwahusisha walimu katika kutatua tatizo la mwanao. Mwanzo wa muhula wa pili uliwapata wazazi hawa afisini mwa naibu wa mwalimu mkuu. Mazungumzo kati ya wazazi, naibu wa mwalimu mkuu na mwalimu wa darasa la Meli yalidhihirisha kwamba walimu walikuwa wamemuasa Meli kuhusu kujiingiza katika makundi yasiyomfaidi lakini rai zao ziliingia katika masikio yaliyotiwa nta. Aliyopenda Zaidi Meli ni shughuli zilizomtoa nje ya shule kama vile tamasha za mziki, ukariri wa mashairi na drama. Mazungumzo yalibainisha kwamba Meli alihitaji ushauri na uelekezaji Zaidi kutoka kwa mtaalamu wa nasaha pale shuleni.
alimpendekezea Meli ushauri zaidi kutoka kwa washauri marika. Hili lilimchangamsha zaidi Meli kwani aliwaona hawa kama wenzake waliojua changamoto zake. Juhudi za mtaalamu wa nasaha na washauri marika zilifua dafu. Mwisho wa kidato cha pili ulishuhudia mabadiliko makuu katika hulka na utendaji kimasomo wa Meli. Aliukata kabisa uhusiano wake na marafiki waliompotosha na kuanza kuandamana na wanafunzi waliotia juhudi masomoni. Polepole alama zake ziliimarika. Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yalimweka kwenye safu ya wanafunzi bora zaidi nchini.
(a) “Wanafunzi wawapo shuleni hukumbana na changamoto nyingi”. Thibitisha ukweli wa kauli hii kwa kurejelea hoja sita kutoka kwenye taarifa. .(alama 6)
(b) Eleza mchango wa washikadau mbalimbali katika kumsaidia Meli kupata ufanisi masomoni. (alama 4)
(c) Bainisha mbinu tatu za lugha ambazo msimulizi anatumia katika kuwasilisha ujumbe wake katika kifungu. (alama 3)
(d)
(i) Andika kisawe cha ‘kijipurukusha’ kwa mujibu wa taarifa (alama 1)
(ii) Andika maana ya ‘kuwatania’ kulingana na taarifa. (alama 1)
UFUPISHO (ALAMA 15)
Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.
Tangu kuripotiwa kwa maambukizi na vifo kutokana na Tandavu la Korona nchini Kenya, Wakenya wengi wamekuwa wakiishi kwa hofu. Vifo vinavyohusishwa na ugonjwa huu hatari vimekuwa vikiongezeka kila kukicha. Ugonjwa huu sugu unawafisha watu kwa muda mfupi baada ya kuambukizwa. Kutokuwepo kwa dawa za kutibu ugonjwa wenyewe kunaongeza wasiwasi miongoni mwa wanajamii. Nchi ya Kenya kama ilivyo mataifa mengine ulimwenguni imehimiza raia wake kupata chanjo dhidi ya tandavu hili. Hata hivyo, hatua ya serikali kutumia vitisho ili kuwashinikiza watumishi wa umma kupata chanjo ya korona haifai kwani huenda ikatatiza mpango wa kuchanja watu milioni kumi mwaka huu. Licha ya serikali kujaribu kuwalazimisha watumishi wa umma bado chanjo haijakubalika na wengi nchini. Kutokubaliwa kwa chanjo hii kumesababishwa na ukosefu wa elimu ya kutosha kuihusu. Watu wengi wanahofia kuwa huenda waliochanjwa wakapata madhara baadaye.
Mamilioni ya watu wameathiriwa kwa njia moja au nyingine na ugonjwa huu. Kenya imeshuhudia hoteli nyingi za kifahari kufungwa. Hii imetokana na usafiri wa ndege kusitishwa kote duniani. Kutokana na hali hiyo, hoteli zilizotegemea wateja watalii zilisimamisha shughuli zake kwa muda. Kwa mfano, ya Intercontinental ilifunga milango yake kabisa mwaka wa 2020. Jambo hili liliwafanya watu wengi kupoteza ajira.
Usafiri wa umma umekumbwa na changamoto si haba kutokana na tandavu la korona. Serikali ilipunguza wasafiri katika magari ya abiria kwa thuluthi moja. Wasafiri hao walilazimika kulipa nauli maradufu kwa safari ile ile. Watu wengi walilazimika kufutilia mbali mipango yao ya usafiri. Kafyu vile vile iliathiri usafiri huu wa umma. Magari mengi yalilazimika kusitisha safari njiani kwa kupatikana na kafyu. Wafanyabiashara katika sekta ya matatu wanahesabu hasara kubwa kwa kukosa abiria. Wengine wamelazimika kuuza magari yao kwa kutamaushwa na changamoto iliyowakumba ghafla.
Aidha, shule zililazimika kufungwa mnamo Machi 2020. Wanafunzi walikaa nyumbani hadi Januari 2021. Hii iliharibu kalenda ya masomo nchini. Serikali ilijaribu kuwasihi walimu kufunza mtandaoni lakini hii haikufaulu hata. Wanafunzi wa kike kadhaa waliishia kupata ujauzito hivyo basi kukatiza masomo yao. Ibada zote pia zilisitishwa. Nao waumini hawakusazwa. Baada ya serikali kufunga makanisa, misikiti na vyumba vingine vya ibada, waumini wengi walilazimika kufuatilia ibada zao katika runinga au mtandaoni. Waliokosa mitandao waliomba na jamaa zao na wengine kupuuza ibada hizo kwa muda.
Shida zilizindikana ugonjwa wenyewe ulipozidi kuenea. Hospitali za umma zililemewa na idadi ya wagonjwa waliokuwa wakienda kule kutafuta matibabu. Vitanda vilijaa na hata wengine wakalala chini katika wadi mbalimbali. Huduma za afya zikazidi kudidimia kutokana na ukosefu wa wahudumu wa afya na vifaa vya kutumiwa na wagonjwa. Vifo vingi vikaripotiwa katika hospitali hizi za umma. Kila sehemu nchini ikaathirika. Majonzi yakajaa kila mahali.
Licha ya haya mabaya yote yaliyokuja na ugonjwa huu wa corona, kuna wale waliochuma riziki kwa kuzuka kwa ugonjwa huu. Mambo mapya yalijitokeza katika ulimwengu wetu. Msamiati wa lugha ukaongezeka. Hii ilitokana na haja ya kuwepo kwa istilahi au misamiati ya kufafanua hali mpya iliyoibuliwa na tandavu hili. Vilevile Kutokana na watu kulazimika kufanya kazi nyumbani, ujuzi wa matumizi ya mtandao umeimarika. Kwa mfano, ufundishaji mtandaoni umefaidi vyuo vingi vinavyofundisha masomo ya mbali.
Wanabiashara wengine wakaanza kuuza barakoa. Barakoa ilikuwa kitu kigeni huku kwetu na duniani kwa jumla. Wengi walipata faida kubwa sana kwa kuwa soko la barakoa lilikuwa pana. Hata hivyo, barakoa zinazotumika na wananchi wengi hazijathibitishwa kuwa bora kuzuia korona. Hali hiyo inawafanya watumiaji wake kuwa na usalama wa bandia kwani wanaweza kuambukizwa ugonjwa wa korona kwa urahisi licha ya kuwa wamevalia barakoa hizo.
Kadhalika, viyeyushi vikaanza kutumika kwa wingi humu nchini na duniani kote. Wachuuzi wengi waliingia biashara hii na kufaidika kiasi. Wengi hawakujua viyeyushi ni nini kabla ya wakati huo. Hivi sasa hata watoto wadogo wanajua viyeyushi na kutumia kwa njia mwafaka.
Kundi lingine lililonawiri kwa korona ni hospitali za kibinafsi. Wengi wa matajiri walioambukizwa ugonjwa huu walijipeleka hospitali hizi kwa matibabu. Wenye hospitali hizo nao wakapandisha bei ya matibabu kwao. Ikawa ni biashara inayonoga kabisa. Hawakujali kuhusu wale wasio na pesa.
Korona imefanikisha juhudi za maafisa wa afya kuhimiza usafi kila mara. Hii ni kwa sababu watu wanalazimika kunawa mikono yao kila mara. Usafi huu wa mikono unapunguza visa vya magonjwa kama vile kipindupindu katika jamii. Aidha, gharama za sherehe zimepungua mno kutokana na sheria za kudhibiti idadi ya watu wanaohudhuria sherehe za mazishi au matanga. Hali hii ni nafuu kwa wale wachochole ambao wakati mwingine hulazimika kuuza kidogo walicho nacho ili kugharamia sherehe za matanga au arusi.
UFUPISHO.
(a) Kwa kuzingatia aya tano za kwanza, eleza shida zilizoletwa na korona. (Maneno 100) (alama 9)
Matayarisho.
Nakala safi.
(b) Fupisha aya nne za mwisho kwa maneno 60. (alama 6)
Matayarisho.
Nakala safi.
MATUMIZI YA LUGHA.
(a) Taja sauti zenye sifa zifuatazo. (alama 2)
(c)Tunga sentensi mbili ili kuonyesha matumizi ya kiakifishi (alama 2)
Vifungo
(d)Tunga sentensi ukitumia: (alama 2)
(e) Ainisha matumizi ya kiambishi “ji” katika sentensi (alama 3)
Jibwa hilo liliweza kujinusuru kutokana na hasira za mkimbiaji.
(f)Andika sentensi ifuatayo katika wakati ujao hali timilifu. (alama 2)
Waziri anasoma hotuba yake.
(g) Tunga sentensi yenye kishazi kirejeshi ambacho ni kivumishi. (alama 2)
(h) Andika sentensi ifuatayo katika hali ya ukubwa. (alama 2)
Nyundo hizo zimetupwa mbali na jumba lile.
(i) Tunga sentensi yenye muundo ufuatao: (alama2)
Nomino ya wingi , kivumishi kiashiria, kitenzi kishirikishi, kielezi cha kiasi jumla’
(j) Changanua kwa vishale: Wale wageni wetu watakuwa wamewasili leo jioni. (Alama 4)
(k) Bainisha yambwa na chagizo katika sentensi inayofuata. (Alama 2)
Vibarua wamefanya hiyo kazi haraka iwezekanavyo.
(l) Badilisha sentensi katika kauli iliyomo kwenye mabano.
(m) Tofautisha matumizi ya ‘Ngali’ katika tungo hizi. (alama 2)
Mama angali mlimani
Otiende angalisoma kwa bidi angaliishi maisha mema.
(n) Andika sentensi katika wakati usiodhihirika ukitumia nomino moja ya jamii. (alama 2)
(o) Ainisha mofimu katika neno lifuatalo (alama 1)
Hakumjia
(p)Tunga sentensi moja kutofautisha maana ya baba na papa (alama 1)
(q) Methali: Haraka haraka haina baraka huambiwa mtu aliye na kasi isiyofaa katika kutenda mambo.Mtu anayepuuza shida za wenzake huambiwa aje? ( Alama 2)
(r) Biwi ni kwa taka ……………………ni kwa maji na kikuba ni kwa ………………. (alama 2)
ISIMU-JAMII
… Bwana Spika, ninaomba kufahamishwa kwa nini Waziri wa Biashara ameshindwa kuchukua hatua kukomesha uuzaji wa vileo hatari kwa watoto wa shule.
(a) Fafanua sifa zozote tano za sajili inayorejelewa na maneno haya (alama 5)
(b)Eleza mambo yaliyochangia msambao wa Lugha ya Kiswahili kabla ya kuondoka kwa wakoloni barani. (Alama 5)